MWINJILISTI QUEEN AWAKUMBUSHA WANAWAKE NEGEZI KUOMBA HAYA MAMBO MUHIMU

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wakristo katika idara ya wanawake kanisa la AICT Negezi lililopo kata ya Masekelo Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kufanya maombi ili mwenyezi Mungu aimarishe ndoa na kubariki familia zao.

Rai hiyo imetolewa leo na Mwinjilisti Queen Stephano wa  kanisa la Mtakatifu Yohana Ndala wakati akihubiri kwenye ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la AICT Negezi Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga.

Amesema kuwa wanawake hawana budi kutumia muda wao kufanya maombi kwaajili ya kuombea familia zao ili ziepukane na matendo yasiyompendeza Mungu.

Mwinjilisti Queen amesema ni muhimu kila mwanamke kutumia hekima na busara katika maisha yao ya  kila siku pamoja na   Ndoa bila kusahau  malezi bora kwa watoto ambayo yatasaidia  kuepusha mifarakano kwenye familia na jamii kwa ujumla.

Aidha Mwinjilisti Queen ametumia fursa  hiyo  kuwakumbusha wakristo kujenga tabia ya kuombeana wao kwa wao huku akiwasisitiza kuombea Taifa hasa vijana kuepukana na mambo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu kama vile  Mapenzi ya jinsia moja ambayo yamekuwa ni chukizo  kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa idara ya wanawake na watoto Kanisa la AICT Local Church ya Negezi Esther Joram amesema idara hiyo imeamua kutumia siku ya leo kuhitimisha  siku ya wanawake ambayo ilikuwa ikienda sanjari na wiki ya akina mama wa Makanisa ya AICT.

Esther amewaomba wanawake wengine kuendelea kuimarisha umoja wao na kwamba ameihidi kuendelea kutoa elimu kwa wanawake wengine ili kuishi katika maisha yenye hekima na maarifa.

Baadhi ya wanawake katika idara ya wanawake Local Church ya Negezi waliohudhuria kwenye ibada hiyo wamesema ushirikiano ni muhimu ili kuimarisha nguvu ya maombi huku wakimpongeza Mwinjilisti Queen kwa mahubiri yake mazuri.

Mwinjilisti Queen Stephano wa  kanisa la Mtakatifu Yohana Ndala wakati akihubiri kwenye ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisa la AICT Negezi Manispaa ya Shinyanga Mkoani Shinyanga.