SHIRIKA LA COWOCE SHINYANGA LATOA ELIMU NA MSAADA WA CHAKULA KWA WANAFUNZI, WAZAZI NA WALEZI WATAKIWA KUTIMIZA WAJIBU WAO

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Shirika lisilo la kiserikali la Mkoani Shinyanga, Companion of Woman and Children Empowerment (COWOCE) limewakumbusha wazazi na walezi kuhamasika na uchangiaji wa chakula cha wanafunzi shuleni ili kuimarisha afya zao.

Akizungumza leo katika zoezi la kuhamasisha wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi shuleni Mkurugenzi  wa shirika la COWOCE Bwana Joseph Ndatala amesema ni muhimu wazazi kuchangia chakula shuleni ili kuwaepusha na magojwa ikiwemo vidonda vya tumbo.

Mkurugenzi Ndatala wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Ndala amewasisitiza wanafunzi hao kwenda kuwaambia wazazi na walezi juu ya umuhimu wa kupata chakula shuleni.

“Utafiti unaonesha wazi kuwa mtoto ambaye amekwenda shule ya awali anafanya vizuri sana shuleni lakini unaambatana na kuwa mtoto anayekula shuleni anafanya vizuri sana darasani kuliko mtoto ambaye hali. Kama mtoto anaingia darasani saa mbili asubuhi mpaka saa 11 jioni hajala kamwe hawezi kumsikiliza vizuri mwalimu”,ameeleza Mkurugenzi Ndatala

“Tumekuja hapa tukiambatana na Vikundi vya COWOCE A na B vinavyosimamiwa na shirika letu la COWOCE linalojihusisha na haki za wanawake na watoto na kuwajengea uwezo wa kujiajiri vijana”.

“Lengo kubwa siyo kuja kutoa msaada bali lengo kubwa sana ni kufikisha ujumbe kwa wazazi wenu na walezi wenu kwamba wana wajibu wa kutoa chakula shuleni. Watoto wengine wapo kwenye mazingira magumu lakini haiwezekani mnakosa hata 1,000/= au 4000/= ya chakula kwa mtoto”,amesema Mkurugenzi Ndatala.

“Hakuna mtoto asiyekula chakula nyumbani, sasa kama watoto wote tunakula chakula nyumbani usiku, naomba tupeleke ujumbe kwa wazazi wachange chakula angalau kidogo kidogo ili muweze kusoma vizuri tupate Mawaziri humu, Wabunge, Madiwani wanaotoka shule zetu kwa sababu chakula kinaongeza afya. Ili tuwe na lishe bora lazima tule chakula”.

 “Hapa tumekuja na chakula kidogo ambacho kwa niaba yenu wanafunzi wachache watapokea hicho chakulaIkiwa ni sehemu ya kuhamasisha utoaji wa chakula shuleni, wazazi watoe chakula na nyinyi watoto msome shule. Pia tunampatia chakula (Mchele kilo 22) mwanafunzi mmoja wa shule ya Sekondari Masekelo kw ajili ya kula shuleni. Hapa katika shule ya Sekondari Ndala tumeleta kilo 30 za mchele”,ameongeza Mkurugenzi Ndatala.

Bwana Ndatala ambaye pia ni Mwenyekiti wa wazazi katika shule hiyo ya Ndala sekondari, ametumia nafasi hiyo pia kuwasihi wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao ambapo pia amewasisitiza kujiepusha na vishawishi vibaya katika safari yao ya masomo.

Aidha shirika la COWOCE kwa kushirikiana na Vikundi vya wanawake wanaojihusisha na ujasiriamali vilivyojengewa uwezo na Shirika hilo wametoa msaada wa vyakula kilo 30 za mchele katika shule ya sekondari Ndala pamoja na kukabidhi kilo 22 za mchele kwa mwanafunzi wa shule ya sekondari Masekelo Vailet Christopha ambaye anaishi katika mazingira magumu.

Wakizungumza kwa niamba ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ndala Alam Petro pamoja na Vailet Christopha mwanafunzi wa shule ya sekondari Masekelo Manispaa ya Shinyanga wamelishukuru shirika la COWOCE kwa kutoa msaada huo.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa COWOCE A, Magdalena Yohana amewakumbusha  wanafunzi hao kumtumaini Mungu katika maisha yao ya kila siku na kwamba wanapaswa kusoma kwa bidii huku wakimtanguliza mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa COWOCE B, Mosi Rashid amewaomba wazazi na walezi kuchangia chakula kwa wanafunzi shuleni ili kuongeza ufaulu kwenye mitihani yao.

Naye Mjumbe wa COWOCE A, Happy Mathias amewasisitiza wanafunzi kuacha kujiingiza kwenye masuala ya mapenzi kwani yanachangia mimba za utotoni na kuathirika kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa upungufu wa kinga mwilini VVU na UKIMWI hivyo amewaomba kujiepusha nayo ili waweze kutimiza ndoto zao.

Akizungumza kwa niamba ya  Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndala, mwalimu wa taaluma  katika shule hiyo Samweli  James amesema ipo changamoto kwa baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika familia zenye mazingira magumu kushindwa kuchangia chakula chao.

Mwalimu James amelipongeza na kulishukuru shirika la COWOCE kwa kutoa msaada huo ambapo amesema chakula hicho kitawasaidia wanafunzi wenye mazingira magumu ambao hawana uwezo wa kuchangia.