Na Mapuli Kitina Misalaba
Mchungaji Charles Lugembe wa Kanisa la AICT Kambarage amewahimiza Wakristo kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza rasmi tarehe 21 Agosti mwaka huu katika Mkoa wa Shinyanga.
Ameyasema hayo leo wakati akisoma matangazo maalum katika ibada ya Jumapili leo Agosti 18,2024 ambapo amewakumbusha wakristo kuwa mfano katika jamii kujitokeza kwenye zoezi hilo ili kuwa na sifa za kuwa mpiga kura halali.
"Kuhusu daftari la mpiga kura, taifa niwajulishe waumini kwamba tumepokea barua ya serikali inasema kuwa tarehe 21 mpaka tarehe 27 zoezi hilo katika Manispaa yetu ya Shinyanga litakuwa linafanyika, hasa wanaohusika ni wale ambao walishaharibu kadi zao na wale ambao wamefika umri wa kuanza kupiga kura, miaka 18, wakapate nafasi ya kujiandikisha wapate kadi ya mpiga kura kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, kwahiyo niwaombe Wakristo ambao mmefikia umri, mkajiandikishe sasa kuna wengine wamepoteza, wengine zimeharibika, basi tuzione ofisi husika kwa ajili ya jambo hilo."amesema Mchungaji Lugembe
Misalaba Media ilizungumza na baadhi ya waumini wa kanisa hilo, ambao wameahidi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo huku wakieleza umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa kujiandikisha wapiga kura kwa maendeleo ya taifa.
Waumini hao wamesisitiza kuwa, kujiandikisha ni wajibu wa kila raia mwenye sifa, ili kuhakikisha wanachangia katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kupitia uchaguzi.
Zoezi la kujiandikisha wapiga kura ni muhimu, hasa kwa wale ambao wamefikia umri wa kupiga kura kwa mara ya kwanza na wale ambao kadi zao za awali zimepotea au kuharibika. Serikali imeweka wazi kuwa zoezi hilo Mkoani Shinyanga litafanyika kwa muda wa siku saba pekee, kuanzia Agosti 21 hadi 27, hivyo ni muhimu kwa wananchi kutumia muda huu kujiandikisha .
Aidha katika mahubiri yake Mchungaji mstaafu wa Kanisa la AICT Ndala, Zabron Mang'wenhula, amewahimiza waumini wa Kanisa la AICT Kambarage kutokata tamaa wanapopitia majaribu na changamoto katika maisha ya Kikristo ambapo amesisitiza umuhimu wa kusaka ushauri wa kiroho na kutafuta msaada kwa viongozi wa kiroho wakati wa majaribu.
"Maisha ya Ukristo yanaweza kuanguka kwenye majaribu, usikate tamaa. Tafuta ushauri, mtafute Yesu, kaa machoni pa Bwana, muombe Bwana, onana na watu wazima wewe kijana, omba ushauri, usikate tamaa," amesema Mchungaji Mang'wenhula
Akiendelea na mahubiri yake, ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa inayokabili jamii na serikali ni kuongezeka kwa visa vya kuvunjika kwa ndoa, jambo ambalo limekuwa likiathiri saikolojia ya wazazi na jamii kwa ujumla huku akiwataka waumini kuwa na subira na kuepuka kuvunja ndoa bila sababu za msingi.
"Serikali yetu inalalamika watu wanavunja ndoa ovyo kwa sababu watu hawakai meza moja na kusameheana niombe vijana wa kanisani masuala ya kuvunja ndoa yawe ni marufuku, kwa sababu mnaharibu saikolojia ya wazazi na mnaharibu saikolojia ya serikali," .
Mchungaji Mang'wenhula amewashauri vijana ambao wanakabiliwa na migogoro katika ndoa zao kutafuta ushauri kutoka kwa viongozi wa kiroho na watu wazima wenye hekima badala ya kuamua kuvunja ndoa. "Kama kuna mgogoro, kwa nini msikae meza moja? Kwa nini msitafute watu wa kuwashauri? Maana tunaowashauri nasaha wengi katika jamii na katika kanisa," amesema.
Wakati huo huo amewatia moyo waumini kwamba ingawa majaribu ni sehemu ya maisha ya kila mmoja, kumkabidhi Yesu Kristo ndiyo njia pekee ya kushinda changamoto hizo.
"Mungu atusaidie sana, majaribu tunaweza tukapata lakini tumkabidhi Yesu Kristo atatushindia na atatutengenezea mlango wa kutokea," amesema.
Mchungaji Charles Lugembe wa Kanisa la AICT Kambarage akiwahimiza waumini wa kanisa hilo kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la kujiandikisha wapiga kura.
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la AICT Ndala, Zabron Mang'wenhula akihubiri kwenye ibada ya leo Jumapili Agosti 18,2024 katika Kanisa la AICT Kambarage.
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la AICT Ndala, Zabron Mang'wenhula akihubiri kwenye ibada ya leo Jumapili Agosti 18,2024 katika Kanisa la AICT Kambarage.
Social Plugin