MKUU wa mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema amewataka madiwani na wakuu wa idara wa halmashauri ya Shinyanga kusimamia vizuri fedha za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kujibu hoja zote zinazotakiwa kujibiwa zikiwa na viambatanisho na zijibiwe kwa wakati.
Pia amesema kila mkuu wa idara anatakiwa ajibu mwenyewe hoja zinazomhusu kulingana na sekta yake, ili aweze kufanya kazi yake kwa usahihi zaidi na kiuadilifu, na hoja zijibiwe kwa wakati kabla hazijapelekwa kwenye baraza la madiwani ndani ya siku 21.
Hayo ameyasema leo kwenye kikao cha baraza la madiwani cha kujadili hoja za CAG, ambapo amesema mara nyingi wakuu wa idara na watumishi wengine hawafanyi kazi zao inavyotakiwa, lakini wakiwa wanajibu wenyewe wanaweza kusimamia kwa uangalifu zaidi tofauti na kuachiwa mzigo wa kujibu halmashauri.
" Kila mkuu wa idara ahakikishe anasimamia ipasavyo fedha zote ambazo zinatolewa kwa ajili ya shughuli ya Miradi ya maendeleo, ili kuepuka mrundikano wa hoja ambazo zinaibuliwa na mkaguzi mkuu wa hesabu (CAG), kwani lengo si kutupiana lawama mnatakiwa kukutana mara moja na kuanza kushughulikia ili kuanza kuzijibu hoja na kuzitatua kwa wakati,"amesema Mjema.
Katibu Tawala wa mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary amewataka watendaji wote wa halmashauri hiyo waajibike zaidi ili wasiwe na hoja nyingi wasikae kusubiri mkaguzi aje ndio waanze kuzifanyia kazi, wakifanya hivyo watapunguza maswali kwenye vikao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ngasa Mboje amewataka wataalamu kuzifanyia kazi hoja za mkaguzi wa ndani kwa kufuata sheria kanuni na taratibu na kufuata bajeti iliyopo pamoja na kutunza kumbukumbu zote zinazotakiwa kutunzwa.
Sonya Jilala diwani wa kata ya Itwangi amesema kwenye hoja nyingi kuna ukosekanaji wa viambatanisho ambavyo ambavyo havionekani vimepotea, mtu anaonekana amelipwa lakini orodha yake haionekani hata kama ameshalipwa, wanashindwa kuelewa kinachoendelea nini.
"Nishauri viambatanisho vyote viandaliwe wakati wa ukaguzi ili tusiendelee kuhoji zaidi na vielelezo vyote vipatikane kwa haraka kwa sababu hata anayelipwa haonekani hata kama amefariki,"tunaomba hili lifuatiliwe"alisema Sonya.
Diwani wa kata ya Ilola Amos Mshandete amesema kuna baadhi ya taasisi hazipo pamoja na halmashauri kwa mfano taasisi ya NHIF haitaki kurudisha fedha za halmashauri, hivyo amemuomba mkuu wa mkoa afuatilie suala hilo ili wasiendelee kuchafua halmashauri.
" Sisi madiwani wa halmashauri tumekuwa tukifuatilia sana lakini hawatusikilizi mkurugenzi wetu amesema atasimamia sheria, lakini na wewe mama yetu tunakuomba ulisimamie suala hili ili fedha zetu ambazo zipo huko NHIF zirudi, kwani hizi hoja hazina majibu, kuna madiwani wengine walianzisha hoja hizi wameshafariki hivyo tunaomba tuwe tunajibiwa kwa usahihi"amesema Mshandete.
Mkaguzi wa hesabu za serikali mkoa wa Shinyanga Anselm Tairo amesema wataendelea kuisihi halmashauri iendelee kufanya ufatiliaji ione jinsi ambavyo hizo fedha zilizoko kwenye taasisi zinarejeshwa yakipatikana majibu na wakionekana watu waliolipwa ama wamefariki wataishauri menejimenti, lakini kwa sasa watanyamaza kwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Nice Munissy alisema maagizo yote yaliyotolewa kwenye kikao hicho yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria pia alisema kikao hicho kimekuwa na mafanikio baada ya kuweza kupata ufafanuzi toka kwenye hoja mbalimbali ambazo ziliibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali hivyo kusababisha hoja nyingi kupata ufafanuzi kwa haraka.
" Pia tunashukuru mwaka huu wa fedha tumefanikiwa kupata hati Safi na hiyo ndiyo lengo ambalo Halmashauri hiyo imejiwekea kusimamia vyema na kudhibiti upotevu wa fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya maendeleo, hivyo tunaamini tutaendelea kufanya vizuri miaka yote na kazi iendelee"alisema Munissy.
Kikao hicho kilikuwa na jumla ya hoja 104 Ikiwa hoja 53 zikiwa ni Mpya zilizoibuliwa na (CAG) na hoja Mpya 51 zikiwa ni hoja za miaka ya nyuma, pia mwaka huu wa fedha halmashauri hiyo wameweza kupata hati Safi na hiyo ndiyo lengo ambalo Halmashauri hiyo imejiwekea kusimamia vyema na kudhibiti upotevu wa fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya maendeleo.
Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary akizungumza.
Social Plugin