WANANCHI WALALAMIKIA UCHELEWESHWAJI WA BARABARA YA KWENDA OLD SHINYANGA, MHANDISI NDIRIMBI AFAFANUA

 Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wananchi na watumiaji wa Barabara ya Uhuru kipande cha Lubaga Old-Shinyanga  wameiomba TANROAD Mkoa waShinyanga kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo ili kuondoa usumbufu kwa watumiaji.

Wamesema ni takribani miezi minne tangu kuanza kwa ujenzi wa barabara hiyo lakini imeshindwa kukamilika huku vifusi vilivyomwagwa vikisababisha usumbufu kwa watumiaji ikiwemo ajali na vumbi linalotishia usalama wa afya za wakazi wa maeneo hayo.

Wamesema kutokamilika kwa wakati kwa barabara hiyo inaathiri biashara zinazofanyika kandokando ya barabara hiyo yakiwemo maduka na shughuli za mama lishe ambao wamedai mazingira hayo yamewakosesha wateja.

Wameishauri serikali kutoa tenda kwa wakandarasi wenye uwezo na vifaa vinavyotosha kutekeleza miradi hali ambayo itasaidia kukamilika kwa wakati kwa ujenzi wa miundombinu.

Mmoja wa wenyeviti wa serikali za mitaa   Bwana Philemon Chikala wa mtaa wa majengo mapya moja ya maeneo unapofanyika uboreshaji wa miundombinu ya barabara ambaye amesema utekelezaji wa miradi hauwashirikishi viongozi wa eneo husika.

Misalaba Blog imezungumza  na meneja wa mamlaka ya udhibiti wa barabara TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi ametaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha kukamilika kwa mradi huo ambapo pia amewaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati huo ambapo juhudi za kukamilisha mradi huo zinaendelea.

“Mradi ule ulianza mwishoni mwa mwezi wa kumi na unatarajia kukamilika mwezi wa sita lakini mradi huo hatutarajii kumalizika mwezi wa sita tunatarajia utakamilika mwanzoni mwa mwezi wa nne”

“Changamoto ambayo ilikuwa ikichelewesha ni kwamba uzalishaji wa ile CRR inatoka nje ya Mkoa na kule ambako inazalishwa kulikuwa na changamoto ya uzalishwaji yale matirio na hiyo mkandarasi alikuwa akitueleza mara kwa mara”.amesema mhandisi Ndirimbi