WAKAZI WA MTAA WA MAGADULA WAIOMBA TARURA SHINYANGA KUTEKELEZA MIRADI KWA UBORA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wakazi wa Mtaa wa Magadula Kata ya Ngokolo katika Manispaa ya Shinyanga wameomba Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini TARURA kutekeleza kwa kiwango chenye ubora miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya barabara.

Wameyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi ambapo pamoja na mambo mengine wananchi hao walibainisha baadhi ya kero ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara isiyokidhi kiwango cha ubora.

Wananchi hao pia wamesema usafi wa mazingira ni jambo linalohitaji juhudi za pamoja na wengine wakalalamikia ufugaji holela unaochangia uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo Bwana Humphrey Mtafungwa ameahidi kuchukua hatua za haraka kushughulikia kero zote zilizopo katika mtaa huo kwa kuwashirikisha TARURA, Ofisi ya Mazingira pamoja na Ofisi ya Afisa Mifugo.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo Kaimu Mtendaji wa Mtaa wa Magadula Bwana Joshua Marco amesema serikali ya mtaa huo imeendelea kutoa elimu ya uraia kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo ushiriki wa wananchi katika kuzuia uhalifu na wahalifu ambapo pia ameagiza kuzingatiwa kwa usafi wa mazingira.

Mwenyekiti wa mtaa wa Magadula Humphrey Mtafungwa  amefanya mkutano wa hadhara kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto za wananchi zilizopo katika mtaa huo.