DC SAMIZI WA SHINYANGA ATAKA WANAWAKE KUFANYA SHUGHULI ZA MADINI KWA UTASHI, TAASISI YA HakiRasilimali YAFANYA KONGAMANO SHINYANGA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Mussa Samizi amewataka wanawake wanaofanya shughuli ya uchimbaji wa madini kufanya kazi hiyo kwa utashi na kujituma ili kuchochea ukuaji wa uchumi imara kupitia sekta hiyo.

Ameyasema hayo wakati akifungua kongamano la wanawake wanaofanya shughuli ya uchimbaji madini mbalimbali kanda ya ziwa ikiwemo gesi asilia  na mafuta ambalo limeandaliwa na taasisi ya HakiRasilimali ambapo DC Samizi amewapongeza wanawake wanaofanya shughuli za madini.

Amesisitiza kuwa ni muhimu wananchi hasa wanawake kuendelea kupewa  elimu sahihi ya uchimbani madini kupitia njia mbalimbali ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara ili waweze kuimarika na kufikia malengo yao.

Dc Samizi amevitaka vikundi vya wanawake wachimbaji wa madini kutumia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani kufanya mabadiliko ya kifikra na kiutendaji kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine zaidi.

“Tufanye kazi yetu akina mama kwa moyo wote na kwa maarifa yote ili shughuli yako isiwe palepale ulipodhani ipande kama ndoto zako zinavyofikiria kwamba siku moja na mimi nitafika pale kwa wale ambao waliogopa kuthubutu mimi nawaambia mthubutu”.

“Nitumie pia fursa hii kupitia  jukwaa hili kuwatakia kheri ya siku ya wanawake wanawake wote wa nguvu na shupavu wote mliopo humu ambao mnapambana na sekta ya madini lakini niwakumbushe tu kwamba usiwe mwezi wa kupendeza, kupaka mekapu, kupaka wanja na poda uwe mwezi wa kubadilika kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine”.amesema DC Samizi

Mkuu huyo wa Wilaya amezitaka taasisi zinazosimamia wachimbaji wa madini ikiwemo tume ya madini pamoja na taasisi ya hakiRasilimali kuendelea kuyaelimisha makundi hayo kuhusu uchimbaji bora na athari zake.

“Waliopewa jukumu la kusimamia sekta ya madini wahakikishe kwamba wanasimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza na zinazoelekeza namna gani ya kuitekeleza Local Content kwa sababu ikitekeklezwa inavyohitajika yale malalamiko ya aki mama sidhani kama tutayasikia tena na kama tutayasikia basi kidogosana”.amesema DC Samizi

Kwa upande wake mtafiti na mchambuzi wa sera kutoka taasisi ya Haki-Rasilimali Bwana Paul Mikongoti ameiomba serikali kuweka msukumo katika ufuatiliaji na usimamizi wa sera na sheria zilizotungwa kusimamia sekta ya madini.

“Tumeshatunga sheria nzuri ambazo zinasimamia sekta yetu na hizo sheria tumeanza kuzitunga toka siku nyingi na tumeziboresha mara nyingi sasa ni wakati wa kuhakikisha kwamba hizi sera na sheria zinatekelezwa kwahiyo turudi tuweke nguvu katika utekelezaji serikali iwe na mkono mrefu katika ufuatiliaji”.amesema Bwana Mikongoti

Baadhi ya wanawake wamempongeza  mkuu wa Wilaya ya Shinyanga ambapo wameahidi kuendelee kufanya kazi kwa bidii ili waweze kufikia malengo yao.

Kongamano la Haki- Rasilimali limefanyika mjini Shinyanga llikijumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini, ikiwemo vikundi vya wanawake wachimbaji wa madini, wataalam kutoka tume na wizara ya madini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Samizi akizungumza kwenye kongamano la wanawake wanaofanya shughuli ya uchimbaji madini mbalimbali kanda ya ziwa ikiwemo gesi asilia  na mafuta ambalo limeandaliwa na taasisi ya HakiRasilimali.