SHIRIKA LA ASMK LATOA MSAADA WA SARUJI NA MAGUDULIA 140 KATIKA SHULE YA BUSIYA- KISHAPU

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Shirika lisilo la kiserikali linaloitwa ANNA SCHUBERT MACKEJA KWOFIE Foundation ASMK limetoa msaada wa Saruji na Magudulia 140 yatakayotumiwa na wanafunzi kwa ajili ya kufuata na kuhifadhi maji

Shirika hilo limetoa magudulia hayo kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wanafunzi kutoka na ndoo nyumbani kwa ajili ya kufuata maji kwenye vyanzo vinavyopatikana umbali mrefu kutoka katika eneo la shule.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi msaada huo,  Mratibu wa utemi wa Busiya Mzee Alfred Muyanga amesisitiza Walimu na wanafunzi kuyatunza magudulia hayo ambayo yatasaidia kuhifadhi maji hivyo kutoa fursa kwa wanafunzi kuhudhuria vipindi darasani.

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Busiya Mwalimu Badi Iddi Mfinanda amepongeza na kusema msaada huo utasaidia kupunguza changamoto zilizopo.

Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Busiya wamelishukuru shirika la ASMK kwa kutoa msaada huo ambao utasaidia kupunguza changamoto zao.

Aidha afisa Elimu  wa kata ya Itilima akizungumza kwa niaba ya afisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Renatus Malima amelipongeza na kulishukuru shirika la ASMK kwa kutoa msaada wa magudulia 140 na saruji katika shule ya sekondari Busiya ambapo amewaomba kuendelea na majitoleo hayo kwa lengo la kuisaidia serikali kutatua changamoto zilizopo.

ANNA SCHUBERT MACKEJA KWOFIE ASMK Foundation ni shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za elimu na maji Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga,ambalo  lipo chini ya himaya ya utemi wa Busiya wa Mtemi Edward Kidaha Makwaia.Mbele upande wa kulia ni mratibu msaidizi wa utimi wa Busiya Bwana Nicholaus Luhende na upande wake wa kulia ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Busiya ambapo nyuma ni viongozi wawakilishi wa shirika la ASMK wakitembelea mazingira ya shule hiyo.

Viongozi wawakilishi kutoka shirika la ASMK ambalo lipo chini ya himaya ya utemi wa Busiya wa Mtemi Edward Kidaha Makwaia, wakikabidhi magudulia hayo kwa wanafunzi na walimu katika shule ya sekondari Busiya.