MWANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA OLD SHINYANGA AFARIKI KWA HITILAFU YA UMEME

Na Mapuli Misalaba, ShinyangaMtoto Rashidi Meshark anayekadiliwa kuwa na  umri wa miaka 14 hadi 15 mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia usiku wa kuamkia Ijumaa baada ya nyumba alimokuwa amelala kuungua kwa moto unaodaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme.

Akitoa taarifa ya tukio hilo Diwani wa Kata ya Old Shinyanga Enock Charles amesema tukio hilo limetokea majira ya saa sita usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa  na kwamba  chanzo chake kimesababishwa na  hitilafu ya umeme

Diwani huyo ameeleza kuwa kwa kkushirikiana na Jeshi la Zimamoto na uokoaji, pamoja na Shirika la Umeme Tanzania TANESCO walifanikiwa kuzima moto huo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Old Shinyanga Bwana Dotto Bwire amesema pamoja na hatua nyingine zilizochukuliwa ilikuwa ni pamoja na kumwahisha kwenye matibabu mtoto huyo ambaye hata hivyo amefariki Dunia akiwa njia kuelekea hospitali.

Misalaba Blog imezungumza na baadhi ya majirani alipokuwa akiishi marehemu Rashidi ambao wameeleza kuwa chanzo cha moto huo kimesababishwa na hitilafu ya umeme na kwamba juhudi za kumwokoa mtoto huyo ambaye alikuwa peke yake ndani ya nyumba hiyo hazikufanikiwa.

 

Wakielezea tukio hilo familia ya marehemu akiwemo mama mzazi wamesema kuwa wakati tukio hilo likitokea mtoto huyo alikuwa peke yake.

 

Mkuu wa Jeshi la zimamoto na uokoaji Wilaya ya Shinyanga Mkaguzi Stanley Luhwago ameeleza kuwa walifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima moto huo kwa kushirikiana na wananchi.

 

Misalaba Blog pia imefika na kuzungumza na Kaimu  Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Leo Mwakatobe ambaye amesema shirika hilo linafanya uchunguzi ili kubaini ukweli wa chanzo cha tukio hilo.

 

Kwa upande wake Dakitari wa kitengo cha dharura katika Hospitali ya Shinyanga Pielina Mwaluko amekili kuupokea mwili wa marehemu huyo majira ya saa sita usiku.

“Majira ya saa sita niliupokea mwili wa marehemu tayari alikuwa ameshafariki, alikuwa ameungua mwili mzima akawa mweusi na tulipomuangalia hakuwa na dalili yoyote ya uhai”amesema Dakitali Pielina