Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Askofu na waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita kwa tukio la kijana wa miaka 25 kudaiwa kuvamia na kuharibu miundombinu ya Kanisa Kuu la jimbo hilo mjini Geita.
Katika salamu zake alizotuma kupitia kwa Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigella, Rais Samia amesema Serikali imesitishwa na tukio hilo la kijana huyo (jina linahifadhiwa) kuvamia na kuharibu vyombo, vifaa na maeneo takatifu ya Kanisa hilo ikiwemo Mimbari (Altare).
“Rais Katuelekeza tuje kutoa pole kwa Askofu, Kanisa na waumini wote kwa kilichotokea; bahati nzuri mtuhumiwa amekamatwa, uchunguzi wa kina utafanyika kubaini kiini na wahusika wote wa tukio hili,” amesema Shigella akiwasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia
RC Shigella amesema anaamini huduma katika Kanisa lililoharibiwa zimesitishwa kwa mujibu wa taratibu za kiimani na kikanisa, na kuahidi kuwa Serikali itashirikiana na uongozi wa Kanisa kuona namna ya kuunga mkono kazi ya kurekebisha miundombinu ya maeneo yote yaliyoharibiwa.
Pamoja na kuharibu Mimbari, kijana huyo anayedaiwa kuingia kanisani hapo baada ya kuvunja kioo cha lango kuu pia alivunja kiti cha Kiaskofu, misalaba, sanamu za kiimani ikiwemo misalaba na vyombo vya kuhifadhia ya maji ya baraka ambayo pia aliyamwaga.
Tukio hilo linalohesabiwa na waumini na viongozi wa Kanisa Katoliki kuwa sawa na kufuru kwa imani lilitokea Saa 8:00 usiku wa kuamkia Jumapili Februari 26, 2023.
Askofu wa Jimbo la Geita, Flavian Kassala ameishukuru Serikali kwa salamu za pole huku akivipongeza vyombo na taasisi za dola kwa kuchukua hatua stahiki ikiwemo kuanzisha uchunguzi wa kina kubaini kiini na wahusika wote wa tukio hilo alilosema kiimani ni kufuru kwa maeeo takatifu.
“Ni matumaini yetu kama Kanisa na Watanznaia kwa ujumla kuona hatua zilizoanza kuchukuliwa (uchunguzi) zitawafikisha kwenye eneo ambalo jamii wataelewa nini hasa kilikuwa nyuma ya mtuhumiwa wa tukio hili,” amesema Askofu Kassala.
Amesema tatizo lililotokea kanisani hapo lina tafsiri na inavuta hisia za kiimani, hivyo ni muhimu kwa vyombo na mamlaka husika kuhakikisha ukweli wa kiini na wahusika unajulikana kwa umma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo unaendelea kwa kumhoji mtuhumiwa ambaye bado anashikiliwa kujua alishirikiana na nani na kwanini alifanya tukio hilo.
Ameiomba jamii kuwa na utulivu na kutoa ushirikiano kufanikisha uchunguzi wa tukio hilo ambalo kwa ucgunguzi wa awali halina uhusiano wowote na chuki kwa Kanisa mtu, taasisi au dhehebu lolote la kidini.
Social Plugin