RICHARD MASHAKA AKUTWA AMEFARIKI NA MWILI WAKE KUTUPWA KICHAKANI MKOANI SHINYANGA




Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa Polisi Janeth Magomi.
                                                  -----------

Kijana mmoja alietambulika kwa jina la Richard Mashaka amekutwa amefariki Dunia na mwili wake kutupwa kichakani kando na makazi ya watu katika mtaa wa Nyihogo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyihogo Iddi Mitimingi amesema alipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa wananchi na alipofika eneo husika walikuta mwili wa kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 28 ukiwa na majeraha.

Tukio hilo limetokea Jumatano Machi 1,2023 majira ya saa moja usiku ambapo Mwenyekiti Mitimingi ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kushirikiana na Serikali ili kukabiliana na matukio hayo.

“nilipigiwa simu na mjumbe wangu muda wa saa moja akanieleza kuwa wamefika kwenye hiyo nyumba ya marehemu walikuta chumba chake kiko wazi na kulikuwa kumeenea damu baada ya hapo nilipofika nikajaribu kuwaambia tuangaze pembeni mwa vichaka hatukufanikiwa asubuhi tukarudi tena”

“Tuliuona mwili wa marehemu akiwa amechinjwa na akiwa amekatwa panga eneo la uso wake ambapo tulimchukua na kumpeleka kituo cha polisi”.amesema Mwenyekiti Mitimingi

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa mtaa huo akiwemo Zawadi Robert pamoja na Leonard Jiritu wameitaka Serikali kushirikiana na wananchi kuimarisha ulinzi shirikishi wa sungusungu kwa ajili ya kuimarisha usalama katika maeneo yao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo,na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo.