DC SAMIZI ATAJA ASILIMIA SHINYANGA WAZAZI WALIOFICHA WATOTO KUCHUKULIWA HATUA KALI

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Samizi amesema serikali itawachukulia hatua wazazi na walezi wa watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Mwaka wa masomo 2023 ambao mpaka sasa hawajaripoti shuleni bila sababu za msingi.

Ameyasema hayo leo wakati akizungumza na Misalaba Blog ofisini kwake ambapo amesema mpaka sasa ni asilimia 91 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga wameripoti shuleni, wakati asilimia 80 katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wameanza masomo.

DC Samizi ametumia nafasi hiyo kuendelea kuwakumbusha wazazi kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa wanaripoti shuleni ili waweze kuendelea na masomo kama ilivyoelekezwa na serikali.

“Mpaka jana Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga tayari wameripoti asilimia 91 kuna asilimia 9 ya watoto bado hawajaripoti shule lakini katika Halmashauri ya Shinyanga vijijini mpaka jana walioripoti ni asilimia 80 kwahiyo kuna asilimia 20 bado hawajaripoti shule lakini serikali ya Mkoa wa Shinyanga imeshatoa maelekezo kwamba hata kama mtoto hana sale mtoto huyo aende shule ili aweze kupata masomo kama wengine”.

Kwahiyo rai yangu ni kwamba wazazi wote ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wahakikishe kufikia jumatatu wiki ijayo watoto hao wawe wamekwenda shule na wanavyozidi kukaa na watoto hao hatua kali zitachukuliwa dhidi yao na sisi tunavyowapa huu muda siyo kwamba hatufuatilii tunatakwimu tunafahamu nani alichaguliwa na nani alikwenda shule ya kulipia”.amesema DC Samizi

Mkuu huyo wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Samizi amesema serikali inaendelea na  juhudi mbalimbali za kuhakikisha wanafunzi hao wanaripoti shuleni wakati wazazi na walezi wakiendelea kukamilisha mahitaji muhimu ya watoto hao ikiwemo sale za shule na vitu vingine.