SERIKALI YATOA MAHINDI WILAYA YA SHINYANGA DC SAMIZI AFAFANUA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Samizi ametoa wito kwa wananchi wote wa Wilaya ya Shinyanga, kununua mahindi yanayouzwa na serikali kwa bei nafuu, ili kukabiliana na mfumko wa bei unaosababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo mtikisiko wa kiuchumi.

DC Samizi ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano maalum na Misalaba Blog ambapo amesema mahindi hayo, yametolewa na serikali kupitia  Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA ili kuwauzia wananchi kwa bei nafuu ya shilingi Mia nane hamsini (850) badala ya shilingi elfu moja mia tano (1500) bei ya sokoni.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Shinyanga Mh. Johari Samizi amesema lengo la serikali ni kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wake unaotokana na sababu mbalimbali ikiwemo mtikisiko wa kiuchumi, na ukame uliosababishwa na mabadiliko ya tabia Nchi,

“Mahindi hayo yametolewa na serikali kupitia ghara la Taifa NFRA na kama mnavyofahamu kwa upande huu wa kanda ya ziwa ghara kuu la NFRA  lipo katika Mkoa wetu huu wa Shinyanga lakini mmeweza kusikia kuna malalamiko ya mfumko wa bei ya chakula lakini pia mmeona hali ya mabadiliko ya tabia Nchi yameathiri swala zima la kilimo”.

“kwahiyo ili kukabiliana na mfumko wa bei serikali ikaona sasa kuwapunguzia wananchi wake ukali wa maisha kwa sababu mahindi hayo kwa bei ya sokoni yanaunzwa kuanzia bei ya 1200 hadi 1500 lakini kupitia mahindi haya ambayo yametolewa na serikali yanauzwa kilo moja kwa bei ya 8500”.amesema DC Samizi

Amewataka  wenyeviti wa mtaa pamoja na watendaji Wilayani Shinyanga  kusimamia zoezi hilo kwa uaminifu na uadilifu ikiwa ni pamoja na kuzingatia bei elekezi ili wananchi waweze kufaidika na fursa hiyo.

Aidha DC Samizi  amewaomba wananchi kutumia fursa hiyo kununua mahindi yaliyotolewa na serikali kwa bei nafuu,ambapo ameonya mahindi hayo yatumike kwa chakula na kwamba  yasibadilishiwe matumizi.