
Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mkoa wa Shinyanga katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa fedha 2022\2023
(Oktoba hadi Disemba Mwaka 2022) ilipokea taarifa za malalamiko 52 zinazohusu
rushwa 23 kutoka kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Afya, maji, elimu pamoja na
serikali za mitaa.
Taarifa hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa TAKUKURU
Mkoa wa Shinyanga Bwana Donasian Kessy wakati akizungumza na waandishi wa
habari ambapo amesema katika kipindi hicho dawati la uchunguzi limepokea
taarifa za rushwa 23 na kwamba uchunguzi wake unaendelea huku taarifa
zisizohusu rushwa ni 29.
Mkuu wa TAKUKURU huyo amefafanua zaidi ambapo
amesema taarifa za rushwa zinazohusu serikali za mitaa 10, Elimu 5, Afya 2,
Maji 2, Mahakama 2, Mazingira moja (1) pamoja na ujenzi taarifa moja (1) ambazo
zote zimeanzishiwa uchunguzi.
Amesema taarifa 29 zisizohusu rushwa upande wa Ardhi
taarifa sita (6), serikali za mitaa 5, Fedha 3, Elimu 3, Polisi 3, Mahakama
kesi moja, Afya kesi 2, Madini kesi 2, Maliasili kesi 2, pamoja na ujenzi kesi
2 ambapo watoa taarifa hizo walishauriwa mahali sahihi pa kupeleka taarifa
hizo.
Mkuu wa
TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amesema taasisi hiyo imefanya
uchambuzi wa mfumo kuhusu uendeshaji wa masoko ya Biashara katika Manispaa ya
Kahama na kubaini kuwa fedha nyingi za serikali zinapotea katika mfumo wa upangishaji
vibanda na meza za biashara kwenye masoko.
“Uchambuzi
wa mfumo kuhusu uendeshaji wa masoko ya biashara katika Manispaa ya Kahama
tulibaini kuna fedha nyingi za serikali zinapotea katika mfumo wa upangishaji
vibanda na meza za biashara kwenye masoko baadhi ya watendaji kwa kushirikiana
na kamati za masoko wamekuwa wakihodhi vibanda na meza kwa kutumia majina ya
wengine na kisha kuvipangisha kwa bei ya juu”.
“TAKUKURU
imebaini uwepo wa wafanyabiashara wapatao 234 katika soko la CDT ambapo
hawalipi kodi au ushuru kwa Manispaa hivyo kuchangia kushuka kwa mapato ya
Manispaa, tumebaini uwepo wa changamoto ya kamati kukusanya ushuru kwa kutumia
risiti za mikono badala ya POS lakini pia tumebaini changamoto ya mikataba
iliyoingia Manispaa juu ya uzoaji wa taka kutojulikana kwa kamati za soko,
TAKUKURU tumebaini pia uwepo wa changamoto za masoko kutokujua kiasi gani cha
bajeti ya Manispaa kinachorudi katika kuboresha miundombinu ya masoko na huduma
nyinginezo katika utendaji wa masoko”. Amesema Kessy mkuu wa TAKUKURU
Mkoa wa Shinyanga
Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian
Kessy amesema hatua mbalimbali zilichukuliwa huku akieleza changamoto
zilizobainika kwenye uchambuzi wa mfumo kuhusu ununuzi na ugawaji wa madawa
Hospitali ya Wilaya, vituo vya Afya pamoja na Zahanati katika Manispaa ya
Kahama.
“Tumebaini
watumishi wa idara ya Afya hawajazi kumbukumbu za ununuzi na ugawaji wa dawa na
vifaa tiba jambo linalosababisha mianya ya rushwa, tumebaini kwenye vituo vya
Afya na Zahanati kuwa na uratibu wa kuazima (Kuomba dawa) hasa vituo vya jirani
ambazo zinachepushwa na wala haziingii katika kumbukumbu lakini pia uwepo wa
madawa yanayoagizwa muda wa matumizi (expiry date) ukiwa umefikia au umekaribia
kufika, TAKUKURU tulibaini MSD kukata fedha baadhi ya vituo bila ya mzigo
husika kufika kituoni na wala invoice kusainiwa vituoni (mzigo hewa), lakini
pia tulibaini kutokuwepo kwa wataalamu wanaojitosheleza katika utoaji wa dawa
na vifaa tiba (kwa maana ya wafamasia na wenye utaalamu wa utunzaji wa dawa)”.amesema
Kessy mkuu wa TAKUKURU Shinyanga
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amesema
katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha kuanzia mwezi Oktoba hadi
Disemba Mwaka 2022 Taasisi hiyo ilijikita kufuatilia fedha za miradi ya
maendeleo ikiwemo sekta ya Afya na barabara ambapo jumla ya miradi ya maendeleo
kumi (10) yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.6 (3,160,000,000) na kwamba
ametaja dosari mbalimbali zilizobainika.
“Tulifuatilia
mradi wa barabara ya mjini inayokwenda Old Shinyanga ambayo inatekelezwa chini
ya usimamizi wa TANROAD mradi huo unathamani ya Shilingi 700,010,000 TAKUKURU
tulibaini kuwa kifusi cha Subgrade layer G15 na Sub base Course G25 (stabilized
with cement) kimelipwa kwa urefu wa 1,080m badala ya 1,000m na kufanya
mkandarasi kulipwa pesa ya ziada ya Shilingi 12,240,000 kwa kazi ambazo
hazijafanyika”.
“Tulibaini
pia hali ya ubora wa barabara ya mchepuko (dirvesion road) siyo nzuri na
inaathiri watumiaji lakini TAKUKURU kuna hatua mbalimbali tulichukua”.ameeleza
mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy
Aidha TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imeridhishwa na
ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari yaliyojengwa mwaka 2022 chini ya
serikali ya awali ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkoa wa Shinyanga ulipatiwa jumla ya Shilingi bilioni
6.6 (6,640,000,000) kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 332 ikiwa ni utekelezaji wa
mradi wa kitaifa wa ujenzi wa madarasa 8,000 ya shule za sekondari ambapo ujenzi
wa madarasa hayo ulitakiwa kukamilika kufikia Disemba 30, 2022.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy
amesema taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa Fedha hizo kwa kutembelea kila
shule iliyopatiwa Fedha ili kuhakikisha Fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa na
miradi inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Amesema TAKUKURU ilifuatilia utekelezaji wa ujenzi
wa madarasa 158 yenye thamani ya Shilingi bilioni 3.1 (3,160,000,000) na kwamba
TAKUKURU haijabaini dosari mpaka sasa ambapo ufuatiliaji bado unaendelea.
Bwana Kessy amesema TAKUKURU imeweka mikakati
mbalimbali ya utendaji kazi kwa kipindi cha Januari hadi Machi Mwaka huu 2023
ikiwemo kuitangaza program ya TAKUKURU – Rafiki iliyoanzishwa na taasisi hiyo
ili kuongeza ushiriki wa kila mwananchi na wadau katika kukabili tatizo la
rushwa ikiwa ni sehemu ya utoaji wa huduma kwa jamii na utekelezaji wa miradi
ya maendeleo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bwana Donansian Kessy
ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa
srikali ili kuhakikisha miradi yote inayoondelea katika Mkoa wa Shinyanga
inakamilika kwa ubora.
“Kama
mtaona kuna vitendo vyovyote ambavyo vinaashiria ubadhilifu wa fedha za miradi
toeni taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa kufika ofisi
zetu zilizopo Shinyanga au piga simu namba 0738150196 au 0738150197, kwa ofisi
ya Kahama piga simu namba 0738150198 na ofisi ya Kishapu piga simu namba
0738150199”.amesema Kessy
TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga inawashukuru wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga hasa wale waliokaribu na maeneo ambapo miradi inatekelezwa kwa kutoa taarifa wanapoona utekelezaji wa miradi unawapa mashaka.
Mkurugenzi wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Bwana Donasian Kessy akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2022\2023
(Oktoba hadi Disemba Mwaka 2022)
Social Plugin