Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya Maji Duniani baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Shinyanga wamepongeza huduma zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga SHUWASA huku wakitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili.
Wananchi hao wametoa pongezi hizo leo wakati wakizungumza na Misalaba Blog kwa nyakati tofauti kuelekea maadhimisho hayo.
Wamesema kuwa wanaendelea kupata huduma ya maji lakini bado zipo changamoto zinazohitaji ufumbuzi ili kuwasaidia wananchi kuendelea kunufaika na huduma hiyo na kwamba wameiomba Mamlaka hiyo kuboresha zaidi huduma ya maji safi na salama kwa wananchi sambamba na kutatua changamoto ya bili za maji.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano na mawasiliano kutoka Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shinyanga SHUWASA, Bi Nsianeli Gerald amewataka watumiaji wa huduma hiyo kutoa taarifa pale inapotokea changamoto ili ishughulikiwe haraka.
Akizungumzia siku ya maji Duniani Bi Nsianeli amesema mamlaka hiyo tayari imefuta faini za wateja waliokatiwa maji na badala yake watalazimika kulipa madeni yao kwa makubaliano.
Kesho ni kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji Duniani ambayo ilizinduliwa rasmi Machi 16, Mwaka huu ikiongozwa na kaulimbiu inayosema “kuongeza kasi ya mabadiliko katika sekta ya maji kwa maendeleo endelevu ya uchumi”.
Social Plugin